Ili kujibu swali hili, ni vyema kurejelea baadhi ya wataalamu ili kupata fasili zao katika kueleza maana ya fasihi.
Oriedo, (2007) anasema kuwa fasihi ni:
Taaluma inayoshughulikia kazi za sanaa zinazotumia lugha kisanii.Wamitila,(2003) anasema kuwa dhana hii ni pana mno ambayo ni vigumu kueleza kwa ufupi. Kulingana naye, ili kufafanua dhana hii ni lazima tutambue kuwa ni
...kazi za kisanaa...zilizotumia lugha kwa usanii na zinazowasilisha suala fulani pamoja kwa njia inayoathiri, kugusa na kuacha athari fulani na kuonyesha ubunilizi na ubunifu fulani na zinazomhusu binadamu.Naye Mogambi, (2008) anadokeza vigezo vitatu vya kuzingatia katika kufafanua fasihi:
Utumiaji wa lugha kisanaa; utungaji wa utungo kutokana na taratibu na hali mbalimbali za maisha; ubunifu (uk111)Kulingana na Bakhressa, (1992) anafafanua fasihi kwa kutolea mifano ya tanzu zake kama vile mashairi, tamthilia
...na mitungo ya sanaa katika lugha.Wataalamu wengine ni Kimani Njogu na Rocha Chimera (2008).Hawa wanasema hivi kuhusu dhana hii:
Fasihi...ni chombo chenye misingi yake katika ubunifu...(ni) aina ya sanaa inayotumia lugha ili kuelezea tajiriba za binadamu.Kutokana na fasili hizi, tunapata mambo matatu makuu yanayoshamiri katika ufafanuzi wa fasihi. Kuwa:
- Fasihi ni kazi ya sanaa
- Lugha ndiyo wenzo mkuu katika kuwasilisha fasihi
- Fasihi huakisi maisha ya binadamu kibunifu
Fasihi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha kibunifu ili kuelezea maisha ya binadamu.
Hii inaashiria kuwa fasihi ni mojawapo tu ya sanaa kama zilivyo uchoraji, uchongaji, ufinyanzi na ususi. Naam, jinsi mfinzanzi atakavyotumia udongo kuumba sanamu kuashiria mtu hodari kama vile Fumo Liyongo ndivyo mchoraji atakavyotumia picha kumchora. Naye mchongaji atatumia mawe au mbao huku mwandishi/ msimulizi akimchora nguli huyo kwa kutumia maneno (ambayo hujenga lugha). Ili kutoa sifa zote alizopewa babe huyo Liyongo, basi msanii wa fasihi lazima atumie ubunifu. Ni ubinifu huu utakaomwezesha kumsawiri mhusika kwa uwazi licha ya yeye kumwona katika ulimwengu halisi.
Fasihi
simulizi :
Maelezo ya wataalamu
mbalimbali ni kama yafuatayo;
Wamitila, (2003)
Fasihi simulizi ni dhana inayorejelea kazi ambazo kimsingi hupokezanwa kwa njia ya masimulizi au kwa mdomo.
Oriedo, (2007) Anaeleza
kuwa:
Hii ni Fasihi ambayo hutumia lugha katika masimulizi. Anaendelea kwa kudokeza kuwa Fasihi hii huhifadhiwa kichwani na kusimuliwa kwa njia ya mdomo ikipokezanwa kutoka kizazi hadi kaizazi.
Mogambi(2008)
Fasihi simulizi ni kazi ya kisanaa inayotumia lugha ya mdomo au mazungumzo katika uwasilishaji wake kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Maelezo haya
yanadhihirisha kuwa utanzu huu wa Fasihi huhusha lugha ambayo hifadhi yake huwa
akilini. Hata hivyo, kuna vitanzu katika Fasihi simulizi ambazo mawasilisho
yake hayahusishi lugha au huwasilishwa kama visaidizi vya kazi husika. Mifano
ya vitanzu hivi ni kama vile matambiko na ngomezi. Vilevile, kudokeza kuwa
Fasihi simulizi ni kazi ya inayotumia lugha katika masimulizi kuna upungufu
wake. Simulizi, kulingana na Wamitila(mtaje) ni;
maelezo kuhusu tukio la uhalisia au la kubuni yanayotolewa na msimulizi mmoja, wawili au zaidi
Hivyo basi hii ina
maana kuwa masimulizi yanaweza kuwa ya kimaandishi au yenye kutolewa kwa njia
ya mdomo. Kutokana na hili basi, kuifafanua dhana hii kwa kuegemea usimulizi
hakutoi kibainishi kamili kati ya Fasihi andishi na Fasihi simulizi. Ni muhimu
basi kueleza dhana hii kwa kuzingatia
vigezo kama vile uwasilishaji na urithi. Kwa mantiki hii basi maana ifuatayo
yaweza kujitosheleza.
Fasihi
Simulizi ni kazi ya sanaa ambayo huwasilishwa kwa njia ya mdomo au kimatendo na
ambayo huhifadhiwa akilini na kupokezwa kutoka kizazi hadi kizazi.
SIFA BAINISHI ZA FASIHI
SIMULIZI
Fasihi simulizi huwa na
sifa zinazoitenganisha na fasihi andishi. Hizi hujitokeza tunapoangazia maswala
kama vile uwasilishaji, ufaraguzi, umilisi, hifadhi, hadhira n.k. Hebu tutazame
kila moja wapo ya sifa hizi.
1.
Uwasilishaji
Uwasilishaji wa kazi
katika huu utanzu huwa kwa njia ya mdomo. Hata hivyo, vipo vitanzu ambavyo
huwasilishwa pasi na kutumia lugha, kama vile ngomezi. Jambo hili hutekelezwa wakati maalum na kwa
hadhira mahususi. Hili linatokana na dhana kuwa vitanzu mbalimbali hutekeleza
majukumu mbalimbali. Kwa mfano, nyiso ni nyimbo zinazoimbwa wakati vijana
wanapopelekwa jandoni au wanapokoshwa unyago. Katika jamii nyingi za Afrika, ni
nadra kupata nyimbo za aina hii zikiimbwa wakati wowote isipokuwa msimu maalum.
Uwasilishaji waweza kuhusisha fanani mmoja au zaidi ya mmoja kutegemea utanzu.
2.
Hadhira
Fasihi simulizi huwa na
hadhira tendi. Hii ina maana kuwa hadhira huwa na uwezo wa kuchangia papo kwa
hapo kazi inapowasilishwa. Kwa mfano, katika usimulizi wa hadithi, fanani
huanza kwa kitangulizi ambacho hunuiwa kujibiwa. Hebu tutazame vielelezo hivi:
i.
Fanani: Hadithi!
Hadithi!
Hadhira: Hadithi njoo!
Fanani: Hapo zamani za…
ii.
Fanani: Paukwa
Hadhira: Pakawa
Fanani: Paliondokea
chanjagaa, kujenga nyumba kaka
Wakati mwingine fanani
huweza kutumia wimbo katikati au kwenye mwisho wa usimulizi. Wimbo huo waweza
kuwa na majukumu yafuatayo;
·
Kuvuta nathari ya hadhira
·
Kuwapumzisha wasikilizaji kutokana na
masimulizi marefu.
·
Kuondoa taharuki hasa katika hadithi za
tanzia.
·
Kushirikisha hadhira katika kazi nzima
ya utambaji.
Aghalabu wimbo huo huwa
rahisi na ambao hadhira wanaweza kujifunza kwa urahisi na hivyo kushiriki
vikamilifu. Kazi nyingine kama vile vitendawili na mafumbo pia huhitaji kuwepo
kwa fanani na hadhira ambayo I tayari kufanya ufumbuzi.
3.
Ufaraguzi
Huu ni uwezo wa fanani
kubadilisha kazi ya Fasihi kwa kutegemea , hadhira, hali na mzingira ambamo
kazi hiyo inatolewa. Kazi
inapowasilishwa kwa hadhira yenye umri mkubwa kama vile kina babu yaweza
kuhusisha mafumbo kwa wingi. Hata hivyo, fanani anapowasilisha kazi ileile kwa
hadhira ya watoto hana budi kubadili lugha ikawa ya wazi. Fanani vilevile
anweza kutumia mbinu kama vile chuku na nyimbo katika kazi ambazo hapo mwanzo
hazikuwa na vipengele hivi. Hii ina maana kuwa Fasihi simulizi hutegemea
pakubwa uwezo wa fanani. Jambo la kuzingatia hata hivyo ni kuwa muwasilishaji
huwa anajizatiti kudumisha maana ya kimsingi iliyokusudiwa.
4.
Umilisi
Fasihi simulizi ni mali
ya jamii. Hakuna yeyote anayeweza kudai
kuwa kazi fulani ni yake. Hii ni kutokana na dhana kuwa utanzu huu huwa
unaelezea historia na maendeleo, desturi na mila za jamii husika. Kwa mfano, unaposikiza
utenzi kama vile “Fumo Liyongo” ni wazi kuwa unapata maelezo kuhusu jamii yake
Nguli huyo. Unaweza kujifunza maswala kama vile ngoma ya gungu na mengineyo
mengi. Mighani mbali mbali kama vile Lwanda Magere hutambulika kwa jamii husika
wala si kwa mtunzi.
5.
Hifadhi
Uhifadhi wa Fasihi
simulizi hutegemea akili za binadamu. Kwa wakati mwafaka, fanani huweza
kuwasilisha anayokumbuka, akaongezea aliyobuni na kuwasilisha kwa hadhira.
Hadhira nayo huhifadhi akilini hadi watakapopata fursa ya kuwa fanani ili
kupokeza kizazi kinachofuata yale waliyopokea. Dhana ya kupokeza kizazi hadi
kizazi ni moja wapo ya sifa muhimu inayotegemea hifadhi na uwasilishaji.
Ikumbukwe hata hivyo kuwa wakati wa sasa zipo kazi ambazo zimehifadhiwa katika
maandishi licha ya kuwa ni kazi za Fasihi simulizi, kwa mfano ni Hekaya za Abunuwasi.
Marejeleo
Bakhressa, K. S. (1992). Kamusi ya Maana na Matumizi. Oxford University Press. Nairobi: Kenya
Mogambi, H. (2008). K. C. S. E. Golden Tips Kiswahili. Macmilan Publishers. Nairobi: Kenya
Njogu, K. na Chimerah, R.(2008). Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Jomo Kenyatta Foundation. Nairobi: Kenya.
Oriedo, E. H. (2007). Istilahi za Fasihi ya Kiswahili. Kenya Literature Bureau. Nairobi: Kenya
Wamitila, K. W. (2003). Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Focus Publications Ltd. Nairobi: Kenya.
+ comments + 1 comments
Good work done. It has helped me a lot.Thank you.
Post a Comment