Katika kazi zozote za sanaa, msanii huwa na msukumo fulani
unaompelekea kutunga au kujenga kazi yake. Msukumo huu huwa ni lengo
kuu linalomwongoza kuiendeleza. Hivyo basi dhamira ya mwandishi huwa
ni lengo linalompelekea
kutekeleza uandishi wake.
Katika Tamthiliya ya Mstahiki
Meya, Mwandishi ananuia
kuusawiri uozo ulio katika uongozi. Hili linadhihirika
kupitia kwa jinsi anavyomchora meya wa Baraza la Cheneo pamoja na
wahusika wengine. Mwandishi anaelekea kuonesha jinsi viongozi huwa
wenye ubadhirifu katika matumizi ya mali ya uma. Kwa mfano, Mstahiki
Meya anasemekana kuwa katika
harakati za kujipatia vipande vya ardhi badala ya kushughulikia
mahitaji ya wananchi. (uk50). Kwamba ametengeneza hela nyingi kwa
muda licha ya kuwa kazi ya
Umeya si ya pato kubwa ni
jambo la kuajabia. Tazama
maongezi haya kati ya Diwani III na Daktari Siki.
Siki: Lazima basi ametengeneza mapeni mengi katika kipindi hiki kifupi cha umeya!Diwani III: Wapi! Umeya hauna pato kubwa. Ofisi ndiyo ina mianya mingi ya kujipatia utajiri...(uk51)
Kutokana na mfano huu, tunaona
mwandishi anavyoelekea
kudokeza kuwa katika afisi za kiserikali, wapo viongozi wanaopunja
mali ya uma wasiulizwe na yeyeyote kwani hata uhalifu unaonekana kuwa
haki.
Vilevile, mwandishi anakashifu
ukosefu wa mwongozo bora
kutoka kwa viongozi wa dini.
Inatarajiwa kwamba wao
watakuwa msitari wa mbele
kupinga uozo katika utawala
wa nchi. Kinyume, Mhubiri
katika mchezo huu anashindwa kutekeleza hilo na badala yake
anamhimiza Mstahiki na hata
kumwombea adumu uongozini (taz uk44).
Baadaye tunaona kwamba anakubali pendekezo la Baraza kumlipia
gharama ya petroli ya usafiri wake pamoja na kuwa Baraza litatoa
sadaka ya shilingi laki moja kila mwezi. Ni wazi kwamba kiongozi huyu
wa dini ni kibaraka wa Meya na kamwe hawezi kumkosoa kwa uongozi wake
mbaya. Kwa hili, mwandishi anaonyesha kushindwa kwa viongozi wa
kidini katika kuirekebisha jamii.
Mwisho, mwandishi anaelekea kusuta
vipengee mbalimbali vya
sheria vinavyowaruhusu viongozi kutekeleza uovu. Haya tunayapata
katika mazungumzo ya Siki na Diwani III
Siki: Sikujua Meya ana uwezo hivyoDiwani III:...Anao tena sana. Kuna Mayor's Act...Kuna sheria nyingine iitwayo Riot Act. Hata akaitumia hii tu inatosha kumkunja kila aliye chini yake kama ua...(uk48)
Baadye
Diwani III anataja jambo lingine kwa jina la Collective
responsibilty. Mwandishi
anatumia vipengee hivi kama mifano ya vifungu mbalimbali katika
katiba za
serikali mbalimbali na
ambavyo viongozi hutumia kuwadhalilisha
wananchi.
Maelezo
haya yanaafiki kuwa mwandishi ameyaona maovu haya katika jamii. Kwa
kuwa fasihi ni kioo cha jamii, amejukumika naye kuweza kuusawiri uozo
huo ili mimi na wewe tuliomo tuweze kubadilika.
Marejeleo
Timothy Arege ( 2011). Mstahiki Meya. Vide-Muwa Publishers Ltd. Nairobi:Kenya
Post a Comment