Translate

UHAKIKI WA TAMTHILIA: KIGOGO

Thursday, September 21, 20170 comments


Anwani: Kigogo
Mwandishi: Pauline Kea
Mchapishaji: Storymoja
Mhakiki: Duncan Were Lutomia
Utanzu: Tamthilia
Kurasa: 94
Bei: KES 377 

Uandishi wa tamthilia kama Sanaa ya maonyesho umefikia upeo wa juu. Kwa muda mrefu, hapajawahi teuliwa kitabu kinachotahiniwa katika shule za sekondari ambacho mwandishi wake ni wa kike! Waandishi wengi waliobobea wameibuka huku kila mmoja akidhihirisha umahiri wake katika taaluma hii. Uteuzi wa Kigogo kama kitabu seti kwa kiwango kubwa kimewapa hadhi waandishi wa kike humu nchini na kuleta usawa katika Sanaa ya uandishi.

Kigogo ni tamthilia iliyogawika katika maonyesho saba(7), na maonyesho hayo yamegawanywa katika matendo kadhaa. Huu ni mtindo sahili na wa kipekee ambao mwandishi ameutumia kuwasilisha kazi yake.

Mwandishi ameangazia na kusawiri mandhari ya jimbo la Sagamoyo ambako mamlaka yote ya nchi yako chini ya Kigogo Majoka na vikaragosi wanaomuunga mkono. Maandhari haya yanaakisi mandhari kamili ya mataifa ya bara la Afrika, panaposhuhudiwa migongano na harakati za ukombozi zinazoendelezwa na wazalendo halisi ili kuleta haki na usawa katika jamii.

Kigogo ni tamthilia inayoelezea kwa ustadi mkuu uozo katika jamii, uongozi mbaya, ukoloni mamboleo na harakati za kuzitetea haki. Mwandishi anaukosoa uongozi mbaya uliopo katika baadhi ya nchi zilizotawaliwa na wakoloni enzi zile. Mengi ya mataifa haya yameeathiriwa na mfumo wa ukoloni mamboleo unaoendelezwa na watawala wenyeji. Huku wakazi wa Sagamoyo wakijiandaa kuadhimisha siku ya uhuru utakaosherehekewa kwa mwezi mmoja na kujivunia maendeleo makuu, soko la Chapakazi, ambalo ndilo tegemeo la wengi linafungwa. Swali ni je, linafungwa kwa nia ipi? Mwandishi pia anatujuza mbinu wanazotumia watawala kuhakikisha kuwa wanasalia madarakani. Kwa mfano utawala wa Majoka- Kigogo, unatumia vitisho, ukandamizaji na hata mbinu ya tenga tawala. Utawala wa nchi nyingi zinazostawi unaonekana ni wa kurithishwa kutoka kwa familia tajika. Majoka anataka kumrithisha mwanawe Ngao Junior utawala pindi tu atakapostaafu. Utawala unakiuka haki za wananchi kwa kuwakandamiza, kwa mfano kulifunga soko la Chapakazi, linalotegemewa na wakazi na wachuuzi kwa riziki yao ya kila siku.

Mchango wa vijana ni muhimu sana katika harakati za ukombozi wan chi kutokana na uongozi dhalimu. Ndivyo anavyodhihirisha Pauline Kea. Vijana ndio viongozi wa kesho hivyo basi wanafaa kupigania haki zao kwa vyovyote vile. Bila shaka Sudi na Tunu wanaajibikia hili.
Mwandishi amewajenga wahusika wake kwa njia halisi inayoakisi jamii za nchi zinazoendelea. Viongozi wanasawiriwa kama wanyanyasaji. Kuna wahusika ambao ni wafuasi kindakindaki wa utawala wa Majoka kwa mfano Ngurumo na walevi wenzake. Kuna wale wanaoupinga utawala wa Majoka kama vile Sudi na Tunu. Wanaoupinga utawala wa Majoka wanajikuta pabaya kwa kuvamiwa (Tunu) na kuumizwa. Hivyo basi baadhi ya wahusika wamezinduka ilhali wengine ni “vipofu’.

Kifani, mwandishi amefaulu sana katika kutumia mbinu za sanaa na tamathali za usemi. Pana matumizi mengi ya jazanda kwa mfano keki ya uhuru, taswira, taharuki, na mbinu rejeshi. Tamathali za usemi ni pamoja na methali, tashbihi, misemo, kuchanganya ndimi n.k. Pia kuna mbinu za uandishi kama vile mdokezo, nidaa, litifati na kuhamisha msimbo. Hili linaongeza ladhaa lugha licha ya kumsisimua msomaji na kurembesha sanaa yake. Aidha mwandishi ametumia mtindo wa kinudhumu ambapo amehusisha nyimbo na mashairi.

Hata hivyo mwandishi ameegemea sana matumizi ya mbinu za uandishi hasa nidaa/kihisishi na mdokezo. Mbinu hizi zinajitokeza kwa wingi hivyo kufinya maudhui.

Licha ya hayo, tamthilia hii imetungwa kwa ustadi mkubwa unaonata msomaji. Bila shaka tamthilia hii ni tunu kwa wanafunzi na wadau wote wa lugha ya Kiswahili!

Bw. Were ni Mwalimu, mlezi na mtetezi wa Lugha ya Kiswahili. Vilevile ni mwandishi wa Diwani ya Mwanga wa Ushairi kwa Shule za Upili  (iliangaziwa katika gazeti la Taifa Leo 29 ,2017 ), mtunzi wa mashairi na mhakiki wa kazi za fasihi.
Share this article :

Post a Comment

 
Usaidizi : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2014. Swahili - Haki zote zimehifadhiwa
Imeundwa na Creating Website Ikachapishwa na Mas Template
Imeletwa kwako na Balozihumu