Translate

Kiswahili ni Kibantu?

Sunday, March 23, 20140 comments


 Kiswahili kilitoka wapi?
Wataalamu wengi wanaelekea kukubali kwamba asili ya Kiswahili inatokana na jamii za Kibantu. Katika utangulizi, Mohammed(2001) kwenye kitabu chake cha Modern Swahili Grammar anasema kuwa:
                              Kiswahili ni milki ya familia kubwa ya lugha za kibantu na
                               inayozungumzwa na takribani watu milioni moja
                              lugha ya kwanza na takribani watu milioni moja...
                                                                               (tafsiri yangu)
Nao Njanje N. and Njogu K. (2006)  kwenye Kiswahili kwa Vyuo vya Ualimu(2006) wanadai kuwa kulingana na isimu, kiswahili ni lugha ya kibantu na waswahili ni waafrika wa kundi la Bantu. Wanasema pia kuwa jina hili 'Swahili' ni jina linalotoka uarabuni lililotajwa kwa mara ya kwanza na Ibn Battuta. Jina hili katika kiarabu linaashiria ubaharia.

Pengine swala la jina hili ndilo linalopelekea watu wengi kufikiri kwamba waswahili ni waarabu. Aidha, wasomi hawa wanasema kuwa jina la jamii iliyotumia lugha hii kuu lilikuwa "Wangozi" lugha yao nayo lugha yenyewe ikiitwa Kingozi.  Ni kutokana na mwingiliano wa kibiashara na ndoa kati ya wangozi na waarabu ambapo jina hilo la Kiswahili lilishamiri na hivo kupoteza tamko la "Kingozi."

Kwa kweli, ni dhana yenye mashiko kwamba lugha ya Kiswahili ina uhusiano mkuu wa kiisimu na lugha za kibantu. Lugha za kibantu, kama ilivyo Kiswahili ni lugha zinazotegemea kabisa uambishi. Uambishaji ni kule kuongeza mofimu  ama kabla, katikati au mwisho wa mzizi wa neno, Habwe J. na Karanja P. (2004). Katika kubadilisha maneno bila kupoteza maana ya kileksia, Kiswahili pamoja na lugha nyingi za kibantu huhitaji mabadiliko katika mofimu hizi. Aidha, katika uambishaji huu kuna hoja ambayo huifanya kiswahili kukaribiana sana na wabantu. Hili ni kwamba haina viambishi vya kati. aghalabu viambishi vinavyotumiwa huwa vya nafsi, wakati, katika hali mbalimbali kama vile ukubwa na udogo, kanushi na yakinishi n.k. Swala hili hujitokeza vivyo hivyo katika lugha nyinginezo za kibantu.

Marejeleo
Habwe J. and Karanja P. (2004) Misingi ya sarufi ya Kiswahili. Phoenix Publishers: Nairobi, Kenya.
 Mohammed, A. M. (2001) Modern Swahili Grammar. East African Educational Publishers: Nairobi, Kenya.
Njanje N. and Njogu K. (2006) Kiswahili kwa Vyuovya Ualimu. The Jomo Kenyatta Foundation: Nairobi, Kenya.
David, P. B. Massamba (). Historia ya Kiswahili. The Jomo Kenyatta Foundation: Nairobi, Kenya.
Share this article :

Post a Comment

 
Usaidizi : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2014. Swahili - Haki zote zimehifadhiwa
Imeundwa na Creating Website Ikachapishwa na Mas Template
Imeletwa kwako na Balozihumu