Ninaenda kwao ng’ambo,
shukurani Mola wangu
Kwa kuyabadili mambo,
na kuondoa uchungu
Walotupigia fimbo,
sasa wametiwa pingu
Siendei misaada,
langu ni kuwafaa tu
Ninaenda kwao ng’ambo,
kuwapatia elimu
Historia na mafumbo,
iliyo barani humu
Na waandishi kiambo,
wa Afrika watadumu
Sitafuti misaada,
langu ni kuwafaa tu
Ninaenda kwao ng’ambo,
nimetazama tuvuti
Ikaninasa ja chambo,
kuona watoto ati
Wanaranda na matumbo,
mitaa wamethibiti
Sitafuti misaada,
langu ni kuwafaa tu
Ninaenda kwao ng’ambo,
kupeleka mausia
Kwamba kwetu hili
jambo, la ndoa twafurahia
Talaka nayo makumbo,
mbali tumetupilia
Sitafuti misaada,
langu ni kuwafaa tu
Ninaenda kwao ng’ambo,
nimewabebea ino
Injili yenye kiimbo,
walioleta kwa wino
‘Mesikia hata nyimbo,
uovu zinao mno
Sitafuti misaada,
langu ni kuwafaa tu
Ninaenda kwao ng’ambo, nimalizapo shairi
Sitabadili msimbo,
nimo ‘wanjani tayari
Enyi weupe ‘warembo,’
ndege sasa naabiri
Sitafuti misaada,
langu ni kuwafaa tu
Post a Comment