Translate

KARANI

Monday, May 12, 20140 comments




Karani ungalijua, machungu yangu maisha
Kwa kweli hiyo barua, niloleta unga'fikisha
Mwenzio ni taabani, kazi natafuta kwisha
Swali nauliza kwako, mbona moyo huna kweli?

Karani miaka mingi, nimo humu vitabuni
Tumaini 'nalo kwingi, ajira tapewa lini
Sitaki kujuta mengi, kumbe nisingesomani
Swali nauliza kwako, mbona moyo huna kweli?

Karani pia kumbuka, wakati ukiisaka
Kwake Mola ukapeka, kukuja'lia kushika
Hayo kusahaulika, wengine kutowataka
Swali nauliza kwako, mbona moyo huna kweli?

Karani ama ni lile, jina langu la pili
'Litambua mara pale, 'kabila langu si hili'
Nilidhani ni ya kale, bado majina ni makali
Swali nauliza kwako, mbona moyo huna kweli?

Karani au pengine, kisomo changu cha juu
Kilifanya ujichune, hulka zako kuu kuu
Uzembeni sipendane, kahofu kuvunjwa 'guu
Swali nauliza kwako, mbona moyo huna kweli?

Karani hebu fikiri, ninaishi kifukara
Kijumba pasi manthari, mazuri si masihara
Jana sikula si siri, sema sina mshahara
Swali nauliza kwako, mbona moyo huna kweli?

Karani mimi mwenyewe, kwa mkuu nilikuja,
Asubuhi leo wewe! Mambo ni kangaja huja,
Wasifu wangu apewe, karidhia zangu hoja,
Swali nauliza kwako, mbona moyo huna kweli?

Karani ujue hasa, naripoti kazi kesho,
Hali ni halisi sasa, mie bosi wako kesho
Nisingependa kisasi, bali nakusihi badilika
Swali nauliza kwako, mbona moyo huna kweli?
Share this article :

Post a Comment

 
Usaidizi : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2014. Swahili - Haki zote zimehifadhiwa
Imeundwa na Creating Website Ikachapishwa na Mas Template
Imeletwa kwako na Balozihumu