1.
Kenya tukichangamka, muovu atatoroka
Hakuna cha kutishika, japo
kunaharibika
Sana tumedhikika, nyoyo zikifadhaika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna
2.
Haiji kukubalika, twaamba pasi na
shaka
Hofu in’otugubika, kwendelea
kutushika
Kwayo tumetosheka, na sasa tumeamka
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna
3.
Imechukua miaka, nchi hii kujengeka
Walianza wahusika, damu ikitiririka
Twalaani umateka, pia damu kumwagika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna
4.
Swali hili linazuka, mataifa tamanika
Huko gaidi watoka, banati wanahusika
Kuwetu hamtafika, sivyo mtabainika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna
5.
Kamwe hatutowaweka, wanasiasa sifika
‘kipata ni washirika, wa makundi ya
vichaka
Afisini watatoka, vizimbani kufungika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna
6.
Wanajeshi mwatukuka, somalia
shughulika!
Watu wengi kaokoka, kwa kazi
ml’ojitwika
Muhimu ni kukumbuka, nyumbani nyuma
yawaka
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna
7.
Tunaweza kulindika, hili jambo
tafanyika
Vikosi kuunganika, usalama imarika
Nyote mkijukumika, sote tutanusurika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna
8.
Viongozi watajika, wa ulinzi hitajika
Si vema kubwekabweka, kwa yale
yasohakika
Mikakati ‘kipangika, idara yenu
tasafika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna
9.
Wananchi matabaka, yoyote hata marika
Tafauti kuz’epuka, ni umoja kujivika
Kila mtu lazimika, jirani kutambulika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna
10.
Hoja zetu zakatika, magotini
twabwagika
Kwako mola twaeleka, maombi
yanatutoka
Rehemazo twazisaka, machafuko
kitapika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna
Post a Comment