Mwishowe Kajwa aliona akibebwa sekaseka. Alitaka kuulizwa walikokuwa wakimpeleka lakini akachelea. Kichapo alichokuwa amepokea kilimtia hofu isiyoelezeka. Dereva aliendesha gari alivyoekezwa. Walifika sehemu moja iliyokuwa na uvundo. Aliona vitoto vilivyoshobweka mashavu. Vingine vilipita na matumbo makubwa na viguu visivyotamanika. Watu wazima walionekana kujibanza kutani kuenda haja ndogo- kina baba na kina mama. Kwa watu wote alioona hakuna aliyekuwa na viatu. Maguo waliyovalia yalikwishaharibika rangi.
Manyunyu ya mvua yaliwanyea. Chini unyevunyevu ulikuwa, tope za rangi nyeusi, hudhurungi na chanikiwiti zilimuudhi Kajwa. Alitezama mbele kidogo na kuona mabanda. Machache yalipisha moshi-ishara ya chajio kuandaliwa. Giza lilianza kuzidi. Kajwa alitetemeka.
"Unaona huu mtaa boss? Hapa ndipo unapofaa kuishi. Kule tulikokutoa hakutembei watu wa simu kamaa hii mkebe yako!"
Alinena Bwana mmoja, pandikizi la mtu huku amemkaba Kajwa shingo. Waliendelea kumuelimisha. Alionywa dhidi ya kutembelea eneo la walalahai na begi nzuri isiyokuwa na pakatalishi. Naam, alielezwa kuwa viatu alivyovaa havikufaa mtu sarafu mbili za shilingi ishirini mfukoni. Walimcheka walipomvua koti na kumwacha na fulana iliyochanika. Fulana hiyo aliinunua miaka minne hapo nyuma alipokuwa chuoni.
"Buda, kwanzia leo utajua kuwa ni makosa kuwa maskini na ni makosa zaidi kudanganya watu kama sisi kuwa una mali. Usingevalia ulivyokuwa tusingekugusa. Una bahati sana. Leo hatukutaka kumwaga damu."
Walimwacha pale akitafakari pa kwenda.Alijiuliza kama majangili hao walijua kuwa kwa kweli hapo walipompeleka palikuwa nymbani kwao.
Aling'angana kukinga vyeti vyake na barua za kazi kutokana mvua hiyo ya vuli. Hata alipotokeza bi kizee mmoja kumsalimu, Kajwa alijipata akijibu, "Umasikini ni kosa."
+ comments + 1 comments
Kazi njema
Post a Comment