Translate

Mbegu

Friday, October 13, 20170 comments

          
Umewahi kuwazia mchakato mzima wa tunda ulipendalo tokea upanzi hadi kinywani mwako? Kweli ni kwamba ni nadra kwetu kuwazia “jambo dogo” kama hili. Labda mawazo kama haya yanaweza kutusaidia pakubwa katika kumaakinika maishani. Chukua kwa mfano embe. Mbegu hupandwa kisha tuvumilie kwa zaidi ya miaka miwili au hata zaidi ili mti ukomae. Kisha tunda litokeze, tena wakati wa majira yake. Kwa vile tuna shughuli nyingi kama vile kusaka matunda ya aina nyingine, hatukai pale tukangojea. Hupendelea tu kulipata mtini tukachuma au sokoni tukanunua.
Mfano huu ndio unijengeao mada ya leo. Je, wewe una maono gani? Yaonekana mazito huwezi kuyafiia au vipi? Nini kinachokuogofya unapoyawazia? Labda ni baadhi ya wenzio waliokuwa na njozi sawia wakashindwa kutimiza?
Ninasisitiza kwamba iwapo maono yako ni ya kitu halisi unachotamania, basi ipo kazi. Katika hali ya kawaida, mtu anapoota ndoto, hawezi kufanya lolote kuathiri vitushi vya ndoto hadi atakapofumbua macho. Hiyo fikra uliyo nayo ni nzuri. Hata hivyo, itabaki palepale usipoifanyia kazi.
Jambo la kwanza ni kunakili unayoyawazia ama kwenye daftari au kwenye tarakilishi. Pili, fanya utafiti. Hatua hii itakufaa kutambua watu ambao wamewahi kufanya hili ulitakalo. Hivyo utaweza kujua njia mwafaka na mbovu ili ukwepe makosa yao. Waaidha, tafuta mawaidha. Ni kweli kwamba dunia ina hadaa. Hata hivyo, wapo adinasi wenye nyoyo safi. Iwapo ni vigumu kwako kumwamini yeyeote basi tumia mtandao kupata ushauri.
Baada ya kupata yote unayohitaji, mwenzangu, changamka. Kama ni uandishi basi anza juzi. Usingoje kesho maanake haifiki abadan katan! Kama ni masomo unda ratiba wakati huu! Kisha uifuate ipasavyo. Kuna baadhi ya miradi ambayo huwa ni vigumu kufanya bila hela. Yaani hukariri methali isemayo ‘mkono mtupu haurambwi.’ Lakini ukumbuke kwamba miradi huenda na hatua. Si hatua zote zinazohitaji hela. Hivyo basi ni vyema kubaini vitengo ambavyo huna upungufu navyo ukaanzia papo hapo.
Tumwekwishafanya utafiti, tukapata habari muhimu na tukaanza utekelezaji. Jambo moja muhimu zaidi ni hili. Je, nyumba unayotaka kujenga ni ya aina gani? Au safari unayokwenda ni ya urefu kiasi gani? Mtu asafirie Sehemu ya kilomita mia tatu halinganishwi na mwenye kwenda kilomita tano. Kulingana na chombo cha usafiri, wawili hawa wanajua kiwango cha subira wanachohitaji.
Maono ni mbegu. Yanahitaji mchanga mzuri, rotuba na mazingira mazuri. Kando na hayo, lazima uwe mvumilivu ili ndoto yako itimie. Katika subra huwa kuna majaribu. Epuka kulalama kila wakati. Waondokee wale wakufishao moyo. Hiyo subra, wamekwishasema wasemao, huvuta heri!


Share this article :

Post a Comment

 
Usaidizi : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2014. Swahili - Haki zote zimehifadhiwa
Imeundwa na Creating Website Ikachapishwa na Mas Template
Imeletwa kwako na Balozihumu