Translate

Sifa Bainifu za Fasihi Simulizi

Friday, March 28, 20141comments

Je, fasihi ni nini? 
 Ili kujibu swali hili, ni vyema kurejelea baadhi ya wataalamu ili kupata fasili zao katika kueleza maana ya fasihi. 
 Oriedo, (2007) anasema kuwa fasihi ni:
Taaluma inayoshughulikia kazi za sanaa zinazotumia lugha kisanii.
Wamitila,(2003) anasema kuwa dhana hii ni pana mno ambayo ni vigumu kueleza kwa ufupi. Kulingana naye, ili kufafanua dhana hii ni lazima tutambue kuwa ni 
...kazi za kisanaa...zilizotumia lugha kwa usanii na zinazowasilisha suala fulani pamoja kwa njia inayoathiri, kugusa na kuacha athari fulani na kuonyesha ubunilizi na ubunifu fulani na zinazomhusu binadamu.
Naye Mogambi, (2008) anadokeza vigezo vitatu vya kuzingatia katika kufafanua fasihi:
Utumiaji wa lugha kisanaa; utungaji wa utungo kutokana na taratibu na hali mbalimbali za maisha; ubunifu (uk111)
Kulingana na Bakhressa, (1992) anafafanua fasihi kwa kutolea mifano ya tanzu zake kama vile mashairi, tamthilia 
...na mitungo ya sanaa katika lugha.
Wataalamu wengine ni Kimani Njogu na Rocha Chimera (2008).Hawa wanasema hivi kuhusu dhana hii:
Fasihi...ni chombo chenye misingi yake katika ubunifu...(ni) aina ya sanaa inayotumia lugha ili kuelezea tajiriba za binadamu.
Kutokana na fasili hizi, tunapata mambo matatu makuu yanayoshamiri katika ufafanuzi wa fasihi. Kuwa:
  • Fasihi ni kazi ya sanaa
  • Lugha ndiyo wenzo mkuu katika kuwasilisha fasihi
  • Fasihi huakisi maisha ya binadamu kibunifu
Hivyo basi tunaweza kusema kuwa:
Fasihi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha kibunifu ili kuelezea maisha ya binadamu.
 
Hii inaashiria kuwa fasihi ni mojawapo tu ya sanaa kama zilivyo uchoraji, uchongaji, ufinyanzi na ususi. Naam, jinsi mfinzanzi atakavyotumia udongo kuumba sanamu kuashiria mtu hodari kama vile Fumo Liyongo ndivyo mchoraji atakavyotumia picha kumchora. Naye mchongaji atatumia mawe au mbao huku mwandishi/ msimulizi akimchora nguli huyo kwa kutumia maneno (ambayo hujenga lugha). Ili kutoa sifa zote alizopewa babe huyo Liyongo, basi msanii  wa fasihi lazima atumie ubunifu. Ni ubinifu huu utakaomwezesha kumsawiri mhusika kwa uwazi licha ya yeye kumwona katika ulimwengu halisi. 




Fasihi simulizi :
Maelezo ya wataalamu mbalimbali ni kama yafuatayo;
Wamitila, (2003)

Fasihi simulizi ni dhana inayorejelea kazi ambazo kimsingi hupokezanwa kwa njia ya masimulizi au kwa mdomo.
Oriedo, (2007) Anaeleza kuwa:
  Hii ni Fasihi ambayo hutumia lugha katika masimulizi. Anaendelea kwa kudokeza kuwa Fasihi hii huhifadhiwa kichwani na kusimuliwa kwa njia ya mdomo ikipokezanwa kutoka kizazi hadi kaizazi.
Mogambi(2008) 
Fasihi simulizi ni kazi ya kisanaa inayotumia lugha ya mdomo au mazungumzo katika uwasilishaji wake kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Maelezo haya yanadhihirisha kuwa utanzu huu wa Fasihi huhusha lugha ambayo hifadhi yake huwa akilini. Hata hivyo, kuna vitanzu katika Fasihi simulizi ambazo mawasilisho yake hayahusishi lugha au huwasilishwa kama visaidizi vya kazi husika. Mifano ya vitanzu hivi ni kama vile matambiko na ngomezi. Vilevile, kudokeza kuwa Fasihi simulizi ni kazi ya inayotumia lugha katika masimulizi kuna upungufu wake. Simulizi, kulingana na Wamitila(mtaje) ni;
maelezo kuhusu tukio la uhalisia au la kubuni yanayotolewa na msimulizi mmoja, wawili au zaidi
Hivyo basi hii ina maana kuwa masimulizi yanaweza kuwa ya kimaandishi au yenye kutolewa kwa njia ya mdomo. Kutokana na hili basi, kuifafanua dhana hii kwa kuegemea usimulizi hakutoi kibainishi kamili kati ya Fasihi andishi na Fasihi simulizi. Ni muhimu basi kueleza  dhana hii kwa kuzingatia vigezo kama vile uwasilishaji na urithi. Kwa mantiki hii basi maana ifuatayo yaweza kujitosheleza.
Fasihi Simulizi ni kazi ya sanaa ambayo huwasilishwa kwa njia ya mdomo au kimatendo na ambayo huhifadhiwa akilini na kupokezwa kutoka kizazi hadi kizazi.

SIFA BAINISHI ZA FASIHI SIMULIZI
Fasihi simulizi huwa na sifa zinazoitenganisha na fasihi andishi. Hizi hujitokeza tunapoangazia maswala kama vile uwasilishaji, ufaraguzi, umilisi, hifadhi, hadhira n.k. Hebu tutazame kila moja wapo ya sifa hizi.
1.      Uwasilishaji
Uwasilishaji wa kazi katika huu utanzu huwa kwa njia ya mdomo. Hata hivyo, vipo vitanzu ambavyo huwasilishwa pasi na kutumia lugha, kama vile ngomezi.  Jambo hili hutekelezwa wakati maalum na kwa hadhira mahususi. Hili linatokana na dhana kuwa vitanzu mbalimbali hutekeleza majukumu mbalimbali. Kwa mfano, nyiso ni nyimbo zinazoimbwa wakati vijana wanapopelekwa jandoni au wanapokoshwa unyago. Katika jamii nyingi za Afrika, ni nadra kupata nyimbo za aina hii zikiimbwa wakati wowote isipokuwa msimu maalum. Uwasilishaji waweza kuhusisha fanani mmoja au zaidi ya mmoja kutegemea utanzu.
2.      Hadhira
Fasihi simulizi huwa na hadhira tendi. Hii ina maana kuwa hadhira huwa na uwezo wa kuchangia papo kwa hapo kazi inapowasilishwa. Kwa mfano, katika usimulizi wa hadithi, fanani huanza kwa kitangulizi ambacho hunuiwa kujibiwa. Hebu tutazame vielelezo hivi:
        i.             
Fanani: Hadithi! Hadithi!
Hadhira: Hadithi njoo!
Fanani: Hapo zamani za…
      ii.             
Fanani: Paukwa
Hadhira: Pakawa
Fanani: Paliondokea chanjagaa, kujenga nyumba kaka
Wakati mwingine fanani huweza kutumia wimbo katikati au kwenye mwisho wa usimulizi. Wimbo huo waweza kuwa na majukumu yafuatayo;
·         Kuvuta nathari ya hadhira
·         Kuwapumzisha wasikilizaji kutokana na masimulizi marefu.
·         Kuondoa taharuki hasa katika hadithi za tanzia.
·         Kushirikisha hadhira katika kazi nzima ya utambaji.
Aghalabu wimbo huo huwa rahisi na ambao hadhira wanaweza kujifunza kwa urahisi na hivyo kushiriki vikamilifu. Kazi nyingine kama vile vitendawili na mafumbo pia huhitaji kuwepo kwa fanani na hadhira ambayo I tayari kufanya ufumbuzi.
3.      Ufaraguzi
Huu ni uwezo wa fanani kubadilisha kazi ya Fasihi kwa kutegemea , hadhira, hali na mzingira ambamo kazi hiyo inatolewa.  Kazi inapowasilishwa kwa hadhira yenye umri mkubwa kama vile kina babu yaweza kuhusisha mafumbo kwa wingi. Hata hivyo, fanani anapowasilisha kazi ileile kwa hadhira ya watoto hana budi kubadili lugha ikawa ya wazi. Fanani vilevile anweza kutumia mbinu kama vile chuku na nyimbo katika kazi ambazo hapo mwanzo hazikuwa na vipengele hivi. Hii ina maana kuwa Fasihi simulizi hutegemea pakubwa uwezo wa fanani. Jambo la kuzingatia hata hivyo ni kuwa muwasilishaji huwa anajizatiti kudumisha maana ya kimsingi iliyokusudiwa.
4.      Umilisi
Fasihi simulizi ni mali ya jamii.  Hakuna yeyote anayeweza kudai kuwa kazi fulani ni yake. Hii ni kutokana na dhana kuwa utanzu huu huwa unaelezea historia na maendeleo, desturi na mila za jamii husika. Kwa mfano, unaposikiza utenzi kama vile “Fumo Liyongo” ni wazi kuwa unapata maelezo kuhusu jamii yake Nguli huyo. Unaweza kujifunza maswala kama vile ngoma ya gungu na mengineyo mengi. Mighani mbali mbali kama vile Lwanda Magere hutambulika kwa jamii husika wala si kwa mtunzi.
5.      Hifadhi
Uhifadhi wa Fasihi simulizi hutegemea akili za binadamu. Kwa wakati mwafaka, fanani huweza kuwasilisha anayokumbuka, akaongezea aliyobuni na kuwasilisha kwa hadhira. Hadhira nayo huhifadhi akilini hadi watakapopata fursa ya kuwa fanani ili kupokeza kizazi kinachofuata yale waliyopokea. Dhana ya kupokeza kizazi hadi kizazi ni moja wapo ya sifa muhimu inayotegemea hifadhi na uwasilishaji. Ikumbukwe hata hivyo kuwa wakati wa sasa zipo kazi ambazo zimehifadhiwa katika maandishi licha ya kuwa ni kazi za Fasihi simulizi, kwa  mfano ni Hekaya za Abunuwasi.



Marejeleo
Bakhressa, K. S. (1992). Kamusi ya Maana na Matumizi. Oxford University Press. Nairobi: Kenya
Mogambi, H. (2008). K. C. S. E. Golden Tips Kiswahili. Macmilan Publishers. Nairobi: Kenya
Njogu, K. na Chimerah, R.(2008). Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Jomo Kenyatta Foundation. Nairobi: Kenya.
Oriedo, E. H. (2007). Istilahi za Fasihi ya Kiswahili. Kenya Literature Bureau. Nairobi: Kenya
Wamitila, K. W. (2003). Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Focus Publications Ltd. Nairobi: Kenya.
Share this article :

+ comments + 1 comments

July 17, 2018 at 2:08 AM

Good work done. It has helped me a lot.Thank you.

Post a Comment

 
Usaidizi : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2014. Swahili - Haki zote zimehifadhiwa
Imeundwa na Creating Website Ikachapishwa na Mas Template
Imeletwa kwako na Balozihumu