Translate

Mstahiki Meya: Dhamira ya Mwandishi

Monday, March 31, 20140 comments


Katika kazi zozote za sanaa, msanii huwa na msukumo fulani unaompelekea kutunga au kujenga kazi yake. Msukumo huu huwa ni lengo kuu linalomwongoza kuiendeleza. Hivyo basi dhamira ya mwandishi huwa ni lengo linalompelekea kutekeleza uandishi wake.
Katika Tamthiliya ya Mstahiki Meya, Mwandishi ananuia kuusawiri uozo ulio katika uongozi. Hili linadhihirika kupitia kwa jinsi anavyomchora meya wa Baraza la Cheneo pamoja na wahusika wengine. Mwandishi anaelekea kuonesha jinsi viongozi huwa wenye ubadhirifu katika matumizi ya mali ya uma. Kwa mfano, Mstahiki Meya anasemekana kuwa katika harakati za kujipatia vipande vya ardhi badala ya kushughulikia mahitaji ya wananchi. (uk50). Kwamba ametengeneza hela nyingi kwa muda licha ya kuwa kazi ya Umeya si ya pato kubwa ni jambo la kuajabia. Tazama maongezi haya kati ya Diwani III na Daktari Siki.
Siki: Lazima basi ametengeneza mapeni mengi  katika kipindi hiki kifupi cha umeya!
Diwani III: Wapi! Umeya hauna pato kubwa. Ofisi ndiyo ina mianya mingi ya kujipatia utajiri...(uk51)


Kutokana na mfano huu, tunaona mwandishi anavyoelekea kudokeza kuwa katika afisi za kiserikali, wapo viongozi wanaopunja mali ya uma wasiulizwe na yeyeyote kwani hata uhalifu unaonekana kuwa haki.
Vilevile, mwandishi anakashifu ukosefu wa mwongozo bora kutoka kwa viongozi wa dini. Inatarajiwa kwamba wao watakuwa msitari wa mbele kupinga uozo katika utawala wa nchi. Kinyume, Mhubiri katika mchezo huu anashindwa kutekeleza hilo na badala yake anamhimiza Mstahiki na hata kumwombea adumu uongozini (taz uk44). Baadaye tunaona kwamba anakubali pendekezo la Baraza kumlipia gharama ya petroli ya usafiri wake pamoja na kuwa Baraza litatoa sadaka ya shilingi laki moja kila mwezi. Ni wazi kwamba kiongozi huyu wa dini ni kibaraka wa Meya na kamwe hawezi kumkosoa kwa uongozi wake mbaya. Kwa hili, mwandishi anaonyesha kushindwa kwa viongozi wa kidini katika kuirekebisha jamii.
Mwisho, mwandishi anaelekea kusuta vipengee mbalimbali vya sheria vinavyowaruhusu viongozi kutekeleza uovu. Haya tunayapata katika mazungumzo ya Siki na Diwani III
Siki: Sikujua Meya ana uwezo hivyo
Diwani III:...Anao tena sana. Kuna Mayor's Act...Kuna sheria nyingine iitwayo Riot Act. Hata akaitumia hii tu inatosha kumkunja kila aliye chini yake kama ua...(uk48)
Baadye Diwani III anataja jambo lingine kwa jina la Collective responsibilty. Mwandishi anatumia vipengee hivi kama mifano ya vifungu mbalimbali katika katiba za serikali mbalimbali na ambavyo viongozi hutumia kuwadhalilisha wananchi.
Maelezo haya yanaafiki kuwa mwandishi ameyaona maovu haya katika jamii. Kwa kuwa fasihi ni kioo cha jamii, amejukumika naye kuweza kuusawiri uozo huo ili mimi na wewe tuliomo tuweze kubadilika.
Marejeleo
Timothy Arege ( 2011). Mstahiki Meya. Vide-Muwa Publishers Ltd. Nairobi:Kenya

 
Share this article :

Post a Comment

 
Usaidizi : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2014. Swahili - Haki zote zimehifadhiwa
Imeundwa na Creating Website Ikachapishwa na Mas Template
Imeletwa kwako na Balozihumu