Translate

UGAIDI TWAUKANA

Thursday, June 22, 20170 comments



Kenya tukichangamka, muovu atatoroka
Hakuna cha kutishika, japo kunaharibika
Sana tumedhikika, nyoyo zikifadhaika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna

Haiji kukubalika, twaamba pasi na shaka
Hofu in’otugubika, kwendelea kutushika
Kwayo tumetosheka, na sasa tumeamka
 Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna

Imechukua miaka, nchi hii kujengeka
Walianza wahusika, damu ikitiririka
Twalaani umateka,  pia damu kumwagika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna

Swali hili linazuka, mataifa tamanika
Huko gaidi watoka, banati wanahusika
Kuwetu hamtafika, sivyo mtabainika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna

Kamwe hatutowaweka, wanasiasa sifika
‘kipata ni washirika, wa makundi ya vichaka
Afisini watatoka, vizimbani kufungika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna

Wanajeshi mwatukuka, somalia shughulika!
Watu wengi kaokoka, kwa kazi ml’ojitwika
Muhimu ni kukumbuka, nyumbani nyuma yawaka
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna

Tunaweza kulindika, hili jambo tafanyika
Vikosi kuunganika, usalama imarika
Nyote mkijukumika, sote tutanusurika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna




Viongozi watajika, wa ulinzi hitajika
Si vema kubwekabweka, kwa yale yasohakika
Mikakati ‘kipangika, idara yenu tasafika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna

Wananchi matabaka, yoyote hata marika
Tafauti kuz’epuka,  ni umoja kujivika
Kila mtu lazimika, jirani kutambulika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna

Hoja zetu zakatika, magotini twabwagika
Kwako mola twaeleka, maombi yanatutoka
Rehemazo twazisaka, machafuko kitapika
Ugaidi twaukana, Kenya nafasi hauna


 https://youtu.be/j7F4IOtS7Kk
Share this article :

Post a Comment

 
Usaidizi : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2014. Swahili - Haki zote zimehifadhiwa
Imeundwa na Creating Website Ikachapishwa na Mas Template
Imeletwa kwako na Balozihumu