Translate

Kwa Mwanangu

Thursday, August 9, 20180 comments



Soma hii kwa makini, ikufae na akili
Nikujuze kwa yakini, maisha mwendo ya mbali
Kufaulu ‘mu duniani, kwataka uwe mkali
Barua naiandika, ikufikie mwanangu

Maono yawe mpini, yashike kila pahali
Jichunge na hayo maoni, yao wasiokujali
Uyachunge hadharani, ubakishe ya muhali
Barua naiandika, ikufikie mwanangu

Anza kushika imani, usiogope kejeli
Nafsi il’o na amani, hupasua majabali
Jishawishi kwa undani, ushindi ni akili
Barua naiandika, ikufikie mwanangu

Ukimpata mwendani, aelewe yako hali,
Mwonyeshane safarini, muwe wenye maadili
Jiepushe  hatarini, msiwe ja mabahili
Barua naiandika, ikufikie mwanangu

Kuna ujinga fulani, ulio kila mahali
Kukaa pale pembeni, na kungoja kazi nzuli
‘Mekaza tai shingoni, ‘kitarajia asali
Barua naiandika, ikufikie mwanangu

Najua pale shuleni, ulitambulika fahali,
Alama zako tisini, hazikukosa kibali
Sasa waona uhuni, walimwengu ni katili
Barua naiandika, ikufikie mwanangu

Ondoka barabarani, uhimize wako mwili,
Vitamu kwa sasa deni, ukisaka raslimali,
Ujijengee maskani, yajayo kihalali
Barua naiandika, ikufikie mwanangu
Picha: Acoustic Moca

Share this article :

Post a Comment

 
Usaidizi : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2014. Swahili - Haki zote zimehifadhiwa
Imeundwa na Creating Website Ikachapishwa na Mas Template
Imeletwa kwako na Balozihumu