Translate

MAISHA MABANDANI

Wednesday, May 21, 20140 comments

Ni madongoporomoka, nakuta nimezaliwa
Vyumba vingi ja vichaka, uvundo nimelaziwa
Popote pale majitaka, pasi unyevu ni chawa
Maisha ya mabandani, ni lini tabadilika?

Chakula si cha kulika,  rangiye ni ya kutisha
Ni sumu hata kwa paka, tena si cha kushibisha
Uhai wetu hakika, ni ule wa ‘bahatisha.’
Maisha ya mabandani, ni lini tabadilika?

Watoto wanapofika, miaka miwili ya’ni
Afiya kuzoroteka, kwetu sio jambo geni,
Bila Mungu kuwaweka, huondoka duniani
Maisha ya mabandani, ni lini tabadilika?

Na tena kuelimika, ni kwa kimiujiza tu
Shule zetu husifika, pengine kwa mabaya  tu
Walimu huwa viraka, mafunzo wachezea tu
Maisha ya mabandani, ni lini tabadilika?

Endea kazi kusaka, kwani umefuzu sasa
Wasifu umeandika, tumaini huwa tasa
Karani naye atamaka, ulilelewa mkasa
Maisha ya mabandani, ni lini tabadilika?

Fununu zinapofika, kule…mjini ku’mwizi
Au mwivi katoroka, washuku sehemu hizi
‘Kachero atatumika, kuchakura makaazi
Maisha ya mabandani, ni lini tabadilika?

Ati ni mtaa duni aka! Ila sikiliza hili
Mabwanyenye wausaka, kutaka kuubadili
Faida si yetu shika, kumbe wanavyo vibali
Maisha ya mabandani, ni lini tabadilika?

Kwa miaka na mikaka, jamii zimesumbuka
                                                 Wakati unaitika, kuwamba ukingo umefika
Tosha! Kudharaulika, sisi ni watu kumbuka!
Maisha ya mabandani, ni lini tabadilika?

Na Balozihumu
Douglas Ogutu
douglasogutu@gmail.com

Share this article :

Post a Comment

Usaidizi : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2014. Swahili - Haki zote zimehifadhiwa
Imeundwa na Creating Website Ikachapishwa na Mas Template
Imeletwa kwako na Balozihumu