Translate

BURUNDI AVUJA

Saturday, December 19, 20150 comments




Haloo mama Afrika, nisemalo walijua
Lakini sikio shika, macho naomba fumbua
Yupo mwana a’yewika, damu yake yasumbua
Burundi avuja

Haloo mama Afrika, wapenda maendeleo
Sasa unashughulika, mikutano ya mazao
Nakusihi nina shuka, umnusuru mwanao
Burundi avuja

Haloo mama Afrika, wapi waumini wako?
Wenye imani kushika, waswali kule waliko
Kwa Mola watasikika, bara lizibe vicheko
Burundi avuja

Nakwita mama Afrika, jiangalie vilivyo
Mambo yanaharibika, hadhiyo yaitwa ovyo
Wasema hujaimarika, kutawala ipasavyo
Burundi avuja


Ewe mamangu Afrika, tia kanga kiunoni
Katili kumsaka, asiyependa amani
Muonye kuheshimika, kwamba hupendi uhuni
Burundi avuja

Haloo mama Afrika,Wito nasema inuka
Familia yaumbuka, vazi lake lachanika
Mbiombio Tanganyika, bila kupumzika
Burundi avuja



Share this article :

Post a Comment

 
Usaidizi : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2014. Swahili - Haki zote zimehifadhiwa
Imeundwa na Creating Website Ikachapishwa na Mas Template
Imeletwa kwako na Balozihumu